Andiko la Kisera: Haki za Wafugaji Waishio katika Eneo la Ardhi Mseto Ngorongoro

 UTANGULIZI

Eneo la Ardhi Mseto Ngorongoro, Tanzania, ni ardhi ya urithi wa wenyeji wa Ngorongoro ambao ni wafugaji wa jamii za Maasai na Barabaig pamoja na wawindaji wa asili wa jamii ya Hadza.

Serikali kushindwa kulinda na kuheshimu haki za wenyeji inachangia kudorora kwa uchumi, mazingira, bioanuai pamoja na hali duni ya maisha ya wenyeji.

Kunahitajika uhifadhi shirikishi unaojali haki za wenyeji pamoja na ikolojia. (pakua nakala ya kijitabu hiki)

Wenyeji wa Ngorongoro kwa zaidi ya miongo sita wamefukarishwa kwa jina la uhifadhi. Andiko hili lina lengo la kubainisha umuhimu wa kubadili hali hii pamoja na kupendekeza mpango endelevu wenye kuendeshwa na ushahidi.

Wenyeji wa Ngorongoro wametengwa kisera na kifedha na kuwa mafukara katikati ya neema. Serikali za kikoloni na hata baada ya uhuru wa Tanganyika na baadae Tanzania zilitunga na zinaendelea kutunga sera na sheria zinazowaonea wenyeji wa Ngorongoro. Sera na sheria hizo zililenga kulinda wanyamapori pamoja na mazingira na hata mali kale katika eneo hilo. Wenyeji wanaonekana kama vile kikwazo huku utalii na uhifadhi vikipendelewa. Haki za wenyeji kunufaika na fedha zinazopatikana katika ardhi yao mara nyingi haikutiliwa maanani. Jitihada nyingi za Serikali ni kuwaondoa wenyeji.

Kuhakikisha kuwa wenyeji wa Ngorongoro wananufaika na ardhi yao ya urithi ni jambo muhimu sana kisera na kiikolojia. Ufukara wa wenyeji kwa vyovyote vile hauwezi kuwa na usalama kiikolojia. Katika miaka ijayo kuna hatari ya Ngorongoro kuangamia endapo wenyeji wataendelea kuwekwa pembeni. Jitahada zao kujikimu kimaisha zitaongeza shinikizo katika eneo zima na hatimaye utalii na uhifadhi kuwa hatarini.

Kuna makubaliano kadhaa ya kimataifa, ambayo Tanzania imekuwa ikiyaongelea kwa maneno matupu bila vitendo, zinazoelekeza kuwa watu wanaoishi katika eneo lenye maliasili nao wanufaike na maliasili hizo. Mikataba na sheria nyingi za Umoja wa Mataifa kama vile Tamko la Umoja wa Mataifa Juu ya Haki za Watu wa Asili (UNDRIP) na Mapatano 169 ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) na nyingine nyingi zimeweka msingi kuwa ni lazima nchi wanachama ziheshimu na kulinda wenyeji pamoja na kuhakikisha kuwa siyo tu wananufaika lakini pia wanaamua wenyewe kuhusu hatima ya pamoja na ardhi na maliasili nyingine zilizoko katika maeneo yao ya urithi.

Tanzania, kama mwanachama wa Umoja wa Mataifa, ni lazima iheshimu matamko, makubaliano pamoja na sera na sheria zinazohusiana na haki za watu wanaoishi katika maeneo yaliyojaliwa maliasili kama vile Ngorongoro kwa manufaa ya wenyeji na taifa.

Historia ya Ngorongoro

Mwaka 1958 Serikali ya Tanganyika chini ya Wakoloni Waingereza ilianzisha Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa kuwahamisha wafugaji kwa nguvu. Baadhi ya wafugaji walihamia Ngorongoro na Loliondo kuungana na wenzao waliokuwa kule.
Wakati Ngorongoro inaanzishwa, wafugaji, ambao wakati huo walikuwa hawalimi na hawali nyama za wanyamapori, waliahidiwa kutumia ardhi yao Ngorongoro pamoja na wanyamapori na watalii. Ngorongoro Conservation Area Act No.14 of 1959, (Cap.284, R.E. 2002) inasema lengo la Hifadhi ya Ngorongoro, pamoja na mambo mengine, ni;

(1) kutunza maliasili
(2) kuendeleza utalii na
(3) “kulinda na kuendeleza maslahi na matakwa ya raia wa Kimaasai, wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanaojishughulisha na ufugaji.”

Wakoloni, pamoja na ukatili wao, waliona huruma na kuahidi kuwa siku za usoni wafugaji hawatohamishwa tena kutoka Ngorongoro. Gavana wa Tanganyika, Richard Turnbull, aliahidi kuwa endapo wafugaji kwa upande mmoja na wanyamapori na watalii kwa upande mwingine watashindwa kuishi pamoja basi wafugaji wabaki Ngorongoro.

Msingi wa hoja hii ni ukweli kuwa wenyeji wa Ngorongoro walipoteza zaidi ya 60% ya ardhi yao ya urithi Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ilipoanzishwa.

Ahadi Zitekelezwe

Pamoja na ahadi kuwa wenyeji wa Ngorongoro hawatohamishwa tena, kwa zaidi ya miaka 60 ya Hifadhi ya Ngorongoro Serikali imeendelea kuwaonea wafugaji. Mwaka 1975 Serikali iliwahamisha kwa nguvu, wafugaji waliokuwa wakiishi ndani ya Bonde la Ngorongoro. Pamoja na makazi kukatazwa ndani ya Bonde la Ngorongoro wafugaji waliruhusiwa kuchunga mifugo yao ndani ya bonde hilo ambalo ni muhimu mno kwa ajili ya nyasi, maji na chumvi chumvi kwa ajili ya mifugo pamoja na wanyamapori.
Pigo la pili kwa wenyeji waishio katika Hifadhi ya Ngorongoro ni kukatazwa kilimo cha bustani kwa ajili ya chakula mwaka 1975. Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Tanzania, John Malechela, aliruhusu kilimo cha kujikimu katika Hifadhi ya Ngorongoro 1992. Mwaka 2001 Waziri Mkuu wa Tanzania, Fredrick Sumaye, alipiga tena marufuku kilimo katika Hifadhi ya Ngorongoro bila kujali kuwa wenyeji wana haki ya chakula. Oktoba 25, 2001 ujumbe wa wafugaji ulikutana na Rais wa Tanzania,

Njaa na UfUkara katikati ya Neema

Kukata malisho ya mifugo katika maeneo muhimu na kupiga marufuku kilimo kumesababisha wenyeji wengi kuwa mafukara wenye njaa ya kudumu. Taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya mwaka 2013 inaonyesha kuwa 97% ya wenyeji wanakabiliwa na njaa. Taarifa ya Tume ya Taifa ya Takwimu ya mwaka 2017 inakiri kuwa kuna ufukara na njaa Ngorongoro. Taarifa ya Tume ya Matumizi Mseto ya Ardhi Ngorongoro ya mwaka pia imebaini kuwa njaa ya kudumu katika Eneo la Ardhi Mseto Ngorongoro.
Utalii katika Eneo la Ardhi Mseto Ngorongoro huingiza zaidi ya Shilingi bilioni 140 kwa mwaka; kabla ya janga la Korona-19. Vile vile kuna uhaba mkubwa wa maji ya kunywa binadamu na mifugo, Ngorongoro. Hoteli na kambi za kitalii huchukua karibu maji yote.
Maendeleo ya wafugaji kama vile kujenga nyumba za kisasa za kuishi, shule na nyumba za ibada yanakatazwa. Ni dhahiri kuwa Serikali ina mkakati wa kuwanyanyasa wenyeji kusudi waondoke wenyewe katika Eneo la Ardhi Mseto Ngorongoro.

Hatima ya Eneo la Ardhi Mseto Ngorongoro

Eneo la Ardhi Mseto Ngorongoro, pamoja na wafugaji kuishi ndani, ndiyo hifadhi inayoongoza kwa kuingizia mapato Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tunapendekeza kuwa wafugaji waachwe wajiendeleze katika ardhi yao ya urithi.
Kama wafugaji kwa upande mmoja na wanyamapori pamoja na watalii kwa upande mwingine hawawezi tena kushamiri katika eneo hili basi wafugaji wabaki Ngorongoro. Pendekezo hili halina athari kubwa kwa wanyamapori kwani Eneo la Ardhi Mseto Ngorongoro ni asilimia 30 pekee ya ikolojia ya Serengeti-Mara iliyohifadhiwa kwa ajili ya wanyamapori na utalii. Hivyo wanyamapori na watalii wataendelea kushamiri.

Wanyamapori wasiruhusiwe kuingia kwenye ardhi ya malisho ya mifugo kwa kuwa mifugo hairuhusiwi hifadhini. Sera hii itapunguza migogoro ya matumizi ya ardhi.

Sera na sheria za uhifadhi nchini ziendane na mikataba na matamko ya kimataifa na ya kikanda ambayo Tanzania imeyaridhia au imetia saini.

Marejeo

Grzimek, B. (1960), Serengeti Shall Not Die, London: Hamish Hamilton Ltd.

Shetler B.J. (2007), Imagining Serengeti: A History of Landscape Memory from Earliest Times to the Present, Athens: Ohio University Press.

Parkipuny, M.S. (1991). Pastoralism, Conservation and Development in the Greater Serengeti Region, London: IIED.

Muhutasari wa Mazungumzo kati ya Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais na Viongozi wa Wilaya ya Ngorongoro yaliyofanyika Dodoma Septemba 17, 1992.

Waziri Mkuu, Fredrick Sumaye, akihutubia mikutano ya hadhara mnamo Septemba 26, 2001 kule Makao, Irkeekpus na Nainokanoka, alipiga marufuku kilimo katika Hifadhi ya Ngorongoro.

Mazungumzo kati ya Mh. Rais Benjamin W. Mkapa na Viongozi wa Mkoa wa Arusha, Mbunge wa Ngorongoro na Wazee wa Kimaasai (Laigwanani) yaliyofanyika Ikulu Ndogo, Arusha, Oktoba 25, 2001.

JMT (2013), Taarifa ya Tathmini ya Watu na Hali ya Uchumi Tarafa ya Ngorongoro, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Dodoma, Septemba.

Rai Septemba 26, 2019.

Download your copy through Ngorongoro Policy Brief Web