HISTORIA YA MAREHEMU MPENDWA WETU
WAKILI EMMANUEL SARINGE NARONYO
TAREHE 22 MACHI 2021
KUZALIWA
EMMANUEL SARINGE NARONYO alizaliwa tarehe 5 Juni 1979 katika Kijiji cha Arash, Wilaya ya Ngorongoro, Mkoa wa Arusha.
ELIMU
EMMANUEL SARINGE NARONYO alisoma Shule ya Msingi Arash kuanzia mwaka 1989 hadi mwaka 1995. Alihitimu Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari Karatu mwaka 1999. EMMANUEL SARINGE NARONYO alisoma Shule ya Sekondari Singe, iliyopo katika Wilaya ya Babati ambapo alihitimu Kidato cha Sita mwaka 2003.
Mwaka 2004 EMMANUEL SARINGE NARONYO alijiunga na Chuo Kikuu cha Tumaini na kutunukiwa Shahada ya Sheria mwaka 2007.
Kati ya mwaka 2008 na 2009 alisoma Shule ya Sheria ya Tanzania. Na hatimaye mwaka 2010 aliapishwa kuwa Wakili wa Mahakama Kuu.
KAZI
EMMANUEL SARINGE NARONYO aliajiriwa na shirika la Wafugaji na Wawindaji wa Asili, PINGO’s Forum, mwaka 2009 kama Mwanasheria wa Shirika nafasi aliyoitumikia kwa uwadilifu na umahiri mkubwa kwa miaka 12 hadi mauti yalipomkuta mwezi huu.
Alifanya tafiti nyingi kuhusu jamii za asili kwa muda wote huo. Vile vile alitoa mafunzo ya sheria mbalimbali katika vijiji vingi hapa nchini.
EMMANUEL SARINGE NARONYO alikuwa mzalendo na ameacha historia ya kiugwa katika utetezi wa haki za ardhi ya jamii za wafugaji na wawindaji wa asili ambapo alishirika katika makongamano mbalimbali ndani na nje ya nchi katika kipindi hicho cha miaka 12.
UGONJWA
WAKILI EMMANUEL SARINGE NARONYO alijisikia vibaya mwanzoni mwa mwezi huu na kushindwa kwenda kazini. Hali yake ilibadilika tarehe 16 Machi 2021 na kupelekwa Hospitali ya Wilaya ya Monduli ambapo alitibiwa hadi mwisho wa maisha yake hapa duniani.
KUFARIKI
WAKILI EMMANUEL SARINGE NARONYO alifariki dunia Monduli tarehe 19 Machi 2021.
FAMILIA
WAKILI EMMANUEL SARINGE NARONYO alioa na Mungu alimjalia watoto wanane (8); wakiume 5 na wakike 3.
SALAMU ZA RAMBI RAMBI
Baadhi ya watu wanaomfahamu EMMANUEL SARINGE NARONYO wanamuelezea kuwa ni mtu mcha Mungu, Msomi na Mcheshi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Wafugaji na Wawindaji wa Asili (PINGO’s Forum), Edward Porokwa, akitangaza kifo hichi alisema;
“Kwa masikitiko makubwa sana nawataarifu kuwa mwenzetu EMMANUEL SARINGE NARONYO amefariki dunia leo mchana katika Hospitali ya Wilaya ya Monduli. Niwape pole sana wote.”
Mwenyekiti wa Bodi ya PINGO’s Forum, Samuel Korinja, anasema;
“Yaani unashindwa kuamini! Mpambanaji mwingine wa haki za binadamu katuacha.”
Katibu Mkuu wa Chama cha Wafugaji Tanzania, Joshua Lugaso, nae kwa majonzi makubwa na huzuni anasema;
“Saringe mbona umeondoka mapema hivi? Umetuachia majonzi. Umeondoka mtetezi wa wafugaji Tanzania. Umetuachia pengo kubwa sana.”
Mheshimiwa Wakili Edward Lekaita, Mbunge wa Kiteto, alisoma darasa moja na EMMANUEL SARINGE NARONYO Chuo Kikuu cha Tumaini (Iringa) na anamuelezea kwa maneno yafuatayo;
“Sijawahi kumuona Wakili Saringe akinuna au kukasirika kwa zaidi ya miaka 16 niliyomfahamu kwa karibu kama rafiki. Alikuwa rafiki mwema na mcheshi.”
Bernard Baha ni Mratibu wa Tanzania Land Alliance. Anasema;
“Tutaendelea kumkumbuka mwenzetu, Wakili Saringe, kwa mchango wake mkubwa sana katika harakati za haki za ardhi na hasa kwa jamii za wafugaji Tanzania.”
Mkufunzi Mwandamizi wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Tumaini (Makumira) Dkt. Elifuraha Laltaika, kwa masikitiko makubwa anasema;
“Wafugaji Tanzania wamepata hasara kubwa mno kutokana na kifo cha EMMANUEL SARINGE NARONYO kwa kweli.”
Juma Mtanda, Mwandishi wa Habari wa gazeti la Mwananchi, anasema;
“Tuna mengi sana ya kusema kuhusu EMMANUEL SARINGE NARONYO. Yatosha tu kusema alikuwa ni mtu mcheshi sana. Tutamkumbuka sana kama mtetezi wa haki za binadamu asieyumba.”
Dkt Lucas Yamat nae alipata bahati ya kufanya kazi na EMMANUEL SARINGE NARONYO. Anamuelezea kwa maneno yafuatayo;
“Kazi za utetezi wa haki za binadamu ni ngumu na hatarishi. Kufanya kazi hii bila kuyumba kama alivyofanya mwenzetu kunahitaji kujitoa. Hakika anahitaji kuenziwa kwa namna ya pekee sana.”
Mika Kusundwa Wamalwa, Mwanaharakati wa Haki za Wafugaji, anaandika kutoka Mkoani Katavi akisema kwa masikitiko;
“Inauma WAKILI EMMANUEL SARINGE NARONYO kuondoka akiwa na umri huo ambao bado ulikuwa unahitajika sana kuitumikia jamii.”
Aline Rabelo ni Mwanafunzi wa Shahada ya Udakitari wa Anthropolojia kutoka Brazil anayesoma Vyuo Vikuu vya EHESS (Ufaransa) na UFRJ (Brazil). Alikutana na WAKILI EMMANUEL SARINGE NARONYO kwa mara ya kwanza mwaka wa 2016, wakati anaanza kufanya utafiti wake wa masomo. Amesikitishwa na msiba huu na kusema;
“Bado siwezi kuamini kwamba umeondoka. Tunashukuru sana kwa urafiki wako na kila ulichofanya kama wakili na mtetezi wa haki za binadamu.”
WAKILI EMMANUEL SARINGE NARONYO ni mfano wa kuigwa kwa jinsi alivyowavutia watoto wa jamii za wafugaji kupenda kusoma. Ana Ndiko ni Mwanasheria mwanamama msomi kutoka Kijiji cha Oloirien katika Wilaya ya Ngorongoro. Anaeleza jinsi WAKILI EMMANUEL SARINGE NARONYO alivyomshawishi kusoma sheria;
“Nikiwa shule ya Msingi nilitamani nisome ili niende Sekondari kama Emmanuel. Enzi hizo sijawahi kuona kijana mdogo ambaye aliamua kumjua Mungu na kuhubiri kama Emmanuel. Alitushawishi kusoma Sheria na tukafanya hivyo kwa mafanikio na bila majuto.”
SHUKRANI
Tunawashukuru sana madaktari, manesi pamoja na wahudumu wengine katika Hosipitali ya Wilaya ya Monduli waliojitahidi kwa kadri walivyoweza kuokoa maisha ya mpendwa wetu WAKILI EMMANUEL SARINGE NARONYO. Shukrani nyingi pia ziwaendee ndugu, jamaa na marafiki ambao kwa moyo wa upendo wamejaribu kwa kadri ya uwezo wao kumsadia na kumtia moyo katika kipindi chote cha ugonjwa na hadi leo kumsindikiza katika nyumba yake ya milele.
BWANA ALITOA, BWANA AMETWAA
JINA LA BWANA LIHIMIDIWE
AMINA!
Unaweza kutazama picha zaidi hapa