TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Katika kipindi kirefu kumetokea na sintofahamu kuhusu hatima ya ardhi ya wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro. Pamoja na mambo mengine Serikali imekuwa ikijaribu namna mbalimbali ya kutatua mgogoro huo wa muda mrefu huku kukiwa na malalamiko kwa wananchi ya kutoshirikishwa na kutishwa pale ambapo wanajitahidi kuuelezea mgogoro huo.
Mnamo tarehe 14 Februari mwaka 2022 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Majaliwa Kassim Majaliwa alitembelea Tarafa ya Loliondo Wilayani Ngorongoro na kuongea na baadhi ya viongozi.
Katika mazungumzo hayo Mh. Waziri Mkuu aliwatoa wasiwasi wananchi na wakazi wa Wilaya ya Ngorongoro kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haina mpango wa kuwahamisha katika makazi yao bali kushirikishana katika utatuzi wa mgogoro, pamoja na hayo ni kuweka mazingira bora ya uhifadhi na kwamba atatuma timu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii kushirikiana na wakazi wa Loliondo kuona namna bora ya kuendeleza eneo hilo kwa maslahi ya umma.
Tamko hilo la Mh. Waziri Mkuu liliwapa matumaini wananchi na wakazi wa Loliondo na Wilaya ya Ngorongoro kwa ujumla kwamba, ardhi yao ipo salama tofauti na ambavyo ilikuwa ikitangazwa na baadhi ya vyombo vya habari, pamoja na mijadala mikubwa Bungeni Jijini Dodoma .
Tarehe 17 Februari 2022 Mh. Waziri Mkuu alikutana na viongozi na wataalam mbalimbali wa uhifadhi kwa lengo la kuongelea changamoto ya uhifadhi kutokana na ongezeko la watu na mifugo ndani ya eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA). Mashirika yasiyo ya kiserikali yalikatazwa kuingia katika eneo la mkutano, na baadhi ya vyombo vya Habari vilitoa malalamiko ya namna hiyo. Licha ya hivyo, wanahabari na dereva mmoja toka shirika lisilo la kiserikali waliwekwa chini ya ulinzi kwa muda wote wa ziara ya Mh. Waziri Mkuu, hali iliyozua wasiwasi na taharuki.
Katika hotuba yake aliweka bayana nia ya kukutana na wadau mbalimbali yakiwemo Mashirika ya Kiraia (NGOs) kwa lengo la kusikiliza maoni yao ili yaweze kusaidia Serikali wakati wa kufanya maamuzi kuhusu mgogoro huo.
Aidha, kumekuwepo na taharuki kwa wenyeji na wakazi wa Wilaya ya Ngorongoro kufuatia taarifa mbalimbali za upotoshaji kupitia baadhi ya vyombo vya habari, mitandao ya kijamii, makundi mbalimbali na mijadala Bungeni.
Sisi Mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) nchini Tanzania kwa umoja wetu tunamshukuru Waziri Mkuu Mh. Majaliwa Kassim Majaliwa kwa kutambua mchango wa Asasi za Kiraia (NGOs) katika utatuzi wa mgogoro huo.
Hakika hili linatia moyo na kutambua shughuli na umuhimu wa kazi zinazofanywa na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) nchini. Kutokana na hili mashirika haya yanaahidi kutoa ushirikiano huu na kumshauri kwa hekima ili maamuzi yanayotarajiwa kufanyika juu ya mgogoro huo, yaweze kuwa kwa maslahi ya kijamii na Taifa kwa ujumla. Pia, maamuzi hayo yaweze kuzingatia utu, haki za binadamu na utawala wa kisheria.
Hivi karibuni kumetokea tetesi kwamba kuna mpango wa kuhakikisha kwamba watakaoruhusiwa kuongea na Mh. Waziri Mkuu wamepandikizwa tayari ili kuhakikisha maoni ya mashirika yasiyo ya kiserikali kutosikika.
Kwa tamko hili, sisi mashirika yasiyo ya kiserikali kwa pamoja tunatoa mapendekezo yetu kwa Waziri Mkuu Mh. Majaliwa Kassim Majaliwa juu ya ushiriki wetu kama ifuatavyo;
- Kwamba, kuna tetesi kuwa kuna watu wanaoandaliwa kuonana na Waziri Mkuu ambao tunaamini hawataleta maoni huru yaliyotokana na umoja wa mashirika yasiyo ya kiserekali. Hivyo, tunatahadharisha kuwa hao hawatakuwa ni wawakilishi wa umoja wa mashirika haya na hivyo maoni yao yachukuliwe kama binafsi nasio kwa niaba ya mashikrika yasio ya kiserikali.
- Kwamba, tunataka uwakilishi wetu tuliouidhinisha katika umoja wetu na pasiwepo na mtu mmoja, wawili au kikundi cha watu watakao toa maoni kama mashirika binafsi bila kuwa sehemu ya umoja wa mashirika haya yasio ya kiserikali kwani huweza kupotosha na kutoa taarifa zisizo sahihi na kupelekea ushauri wa Serikali kutokuwa na mashiko katika kutoa usuluhishi wa mgorogoro kusudiwa juu ya wenyeji wa Tarafa za Sale, Loliondo na Ngorongoro.
- Kutokana na uzito wa jambo hili, Waziri Mkuu Mh. Majaliwa Kassim Majaliwa atoe muda wa kutosha kwa mashirika katika kipindi cha mazungumzo na mashauriano ili kuwezesha upatikanaji wa maoni mengi na mapendekezo wa namna bora ya kutatua mgogoro wa Wilaya ya Ngorongoro. Pia kuwezesha serikali kupata muda wa kuchambuwa na kutoa maamuzi stahiki kwa maisha ya wenyeji wa Wilaya ya Ngorongoro na Taifa zima.
- Kwamba Mh. Waziri Mkuu atoe maelekezo kwa wasaidizi wake pasiwepo na vitisho, uzuiaji wa kuingia katika eneo la mkutano kwa makundi mbalimbali ikiwemo waandishi wa habari hususani wa vyombo vya habari binafsi, waandishi wa kujitegemea na Mashirika yasiyo ya kiserikali.
- Tunalaani nia ovu ya kupandikiza ushiriki wa baadhi ya wadau ambao kusudi lao si la kufanikisha suluhu inayotenda haki.
Tunashauri serikali iwe na dhamira chanya ya kuweka milango wazi pale ambapo panahitajika kupata ushauri toka mashirika yasiyo ya kiserikali na vilevile pale ambapo mashirika yasiyo ya kiserikali yatahitaji kuwasilisha maoni au hoja zao serikalini.
Tamko hili limetolewa leo tarehe 25 Februari, 2022 na mashikirika yafuatayo;
- Tanzania Land Alliance – TALA
- Haki Ardhi
- Arusha Non- Governmental Organization Network – ANGONET
- Pastoralist indigenous Non-Governmental Forum – PINGOs Forum
- Tanzania Human Rights Defenders Coalition – THRDC
- Ujamaa Community Resource Team – UCRT
- Pastoral Women’s Council – PWC
- Pastoral Livelihood Support and Empowerment Programme – PALISEP
- Integrated Development Initiative in Ngorongoro – IDINGO
- Tanzania Natural Resource Forum – TNRF
- Community Research Development Services – CORDS
- Laretok- Le-sheria na Haki za Binadamu Ngorongoro – LASHEHABINGO
- OSEREMI Integral Development Association
- Civic and Legal Aid Organization – CILAO