Ikiwa ni siku ya pili ya mkutano wa kimataifa wa Umoja wa Mataifa kuhusu mazingira na mabadiliko ya tabia nchi, dunia imeaswa kusikiliza jamii za asili kutokana na uelewa wao na maarifa ya asili ambayo huwapa kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya tabia nchi.
katika mahojiano na BBC Swahili, mratibu wa mabadiliko ya tabia nchi PINGO’s Forum, Gideon Sanago, ameelezea kuwa dhana ya wafugaji kuachana na mfumo wao wa maisha ni kitu kisichowezekana, kama ilivyo kwa baadhi ya wazungu kutoweza kuishi bila ‘pizza’ ama ‘burger’
“Tumebeba sauti kubwa ya jamii za wafugaji wa Kimaasai, Wabarbaig na wahadzabe [wakusanya matunda] Tanzania, kuleta kilio kwa wakubwa wa dunia ambao wamekusanyika hapa, akiwepo Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan, ambaye naye vilevile ameleta kilio cha Watanzania ambao wameathirika na mabadiliko ya tabia nchi. Kwa upande wetu sisi tumekuja kuhakikisha kwamba tunatoa mchango wetu namna gani sehemu kubwa ya maarifa ya asili tuliyonayo, inaweza ikatumika kwenye tafiti mbalimbali zinazofanywa na Umoja wa Mataifa – ili kusudi kuiokoa dunia na mabadiliko ya tabia nchi”
Gideon ameongeza kuwa wanataka kuwa rafiki na sehemu ya sera mbalimbali na mikakati inayotengenezwa kwenye mkutano huo ili wapate kunufaika kama jamii za pembezoni. Aidha Gideon alimalizia kwa kueleza namna ambavyo mfumo wa maisha wa jamii za asili ulivyo rafiki na mazingira – ukiwa na misituya kutosha ikiwemo wanyamapori ambao hujihisi salama wakiwa maeneo ya jamii hizi.
Unaweza kutazama kipindi chote kwa kubofya hapa.