Hatimaye Marais Dkt. Jakaya Kikwete na Dkt. Ali Shein wamepokea Katiba inayopendekezwa kutoka Bunge Maalum la Katiba, ambalo limemaliza kazi ya kujadili Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania – kama ambavyo ilikabidhiwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Katika kuikabidhi Katiba hiyo, wawakilishi wa makundi tofauti wameelezea ibara kadhaa ambazo zinawapa manufaa na kuitaka jamii iipokee kwa mikono miwili, Huku aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Samueal Sitta, akiisifia kuwa Katiba yenye viwango. Iwapo itapita, basi itaitwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (JMT) ya mwaka 2014. Ikichukua nafasi ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ambayo ndio inatumika hadi sasa.
Kinachosubiriwa kwa wakati huu ni ratiba ya kura ya maoni, ambapo wananchi wataamua kama Katiba iliyopendekezwa inawafaa ama vinginevyo, yaani ‘Ndio ama Hapana’.