Tamko la Makundi ya Wafugaji Kumpongeza Rais Magufuli

TAMKO LA MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI NA VIONGOZI KUTOKA MAKUNDI MBALIMBALI YA WAFUGAJI LA KUMPONGEZA MH. RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA DK.JOHN JOSEPH POMBE MAGUFULI
LEO TAREHE 16/1/2019

MOUNT MERU HOTEL

1.0 UTANGULIZI:

Ndugu Wanahabari tumewaita hapa kwa  niaba  ya wafugaji  nchini  kama mashirika yanayotetea haki za wafugaji pamoja  na viongozi  wa  makundi mbalimbali ya wafugaji nchini kwa nia ya dhati  kabisa ya kumpongeza  Mh. Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa maagizo na maelekezo aliyoyatoa  jana  tarehe  15/1/2019 akiwa  IKULU – Dar es Salaam.

Tamko la Mheshimiwa Rais kwa vyombo vya Habari kupitia Kurugenzi ya Mawasiliano IKULU limeweka bayana kuwa Mh. Rais anachukizwa sana kuona wafugaji wanafukuzwa kila mahala katika maeneo ya vijiji na vitongoji vinavyopakana na maeneo ya Hifadhi.

Mhe. Rais pia ameweka bayana na kuwataka viongozi wote wa serikali wakae na kutanguliza maslahi ya wananchi (wafugaji) katika kuhakikisha kuwa hakuna kijiji au kitongoji kilichoainishwa kuwepo katika maeneo ya hifadhi kitakachoondolewa.

Ndugu wanahabari, wafugaji nchini kwa muda mrefu  sana  wamekuwa wakipata taabu na changamoto nyingi zinazotokana na kuondolewa kwa nguvu wakati mwingine kuharibiwa mali zao kwenye maeneo yao ambayo wamekuwepo kwa muda mrefu kwa kisingizio kuwa ni maeneo ya hifadhi.

Ndugu wanahabari ni’ ukweli usiopingika kuwa maeneo mengi nchini yanapakana na maeneo ya Hifadhi za Taifa na hivyo ni majirani wema na wapenda uhifadhi. Lakini kwa muda mrefu wafugaji wengi nchini wamekuwa wanateseka kutokana na adha kubwa wanayopata kutokana na kuondolewa na kufukuzwa katika maeneo yako kila wakati na kila pahala.

Sisi kama mashirika na viongozi wa wafugaji nchini tunazo taarifa nyingi za unyanyasaji wa wafugaji katika maeneo yao ambayo yamemegwa na hifadhi,­ kufukuzwa kwa wafugaji katika maeneo haya kwa muda mrefu na kila wakati imejenga taswira mbaya kwa wafugaji kuhusu maswala ya uhifadhi unafanywa na vyombo vinasimamia maeneo haya bila weledi.

Ufukuzwaji wa wafugaji katika maeneo haya umekuwa unafanywa kwa nia mbaya na wakati mwingi, wafugaji kuchomewa mali zao, kutaifishwa mifugo na mali zao, kutozwa faini za ajabu na kukamatwa hovyo na kufunguliwa kesi na kuteswa bila huruma.

Ndugu wanahabari, ninyi ni mashahidi wa changamoto lukuki walizopata wafugaji katika maeneo yao ambayo yapo karibu au kupakana na maeneo ya hifadhi chini. Uonevu huo ambao umekuwa unafanywa dhidi ya wafugaji katika maeneo yanayopakana na maeneo ya hifadhi umepelea wafugaji kuonekana kama wakimbizi katika nchi yao na wakati  mwingine kujenga taswira mbaya kuhusu wafugaji katika maswala ya uhifadhi na utunzwaji wa mazingira.

 

2.0   SABABU ZA KUMPONGEZA MHESHIMIWA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

2.1 Tumekutana hapa kwa nia ya dhati kabisa ya kumpongeza Mhe. Rais kwa kuyatambua vyema matatizo na manyanyaso makubwa ambayo wafugaji wamekuwa wakiyapata katika maeneo yao yanayopakana na maeneo ya uhifadhi. Changamoto ambazo wafugaji wamekuwa wakizipata kwa muda mrefu.

2.2 Tumekutana hapa kwa kumpongeza Mhe. Rais kwa kutoa maagizo kwa vyombo vya serikali hususan wizara ya maliasili na utalii na kuwataka kuhakikisha kuwa hakuna mfugaji atakayeondolewa katika kijiji au kitongoji chake vilivyoainishwa kuwa katika maeneo ya uhifadhi.

2.3 Tumekutana kumpongeza Mhe. Rais kwa kuweka wazi bila kuficha kuwa anachukizwa sana kuona wafugaji wanafukuzwa kila mahali.

2.4 Tumekutana hapa kumpongeza Mhe. Rais kwa kuwaagiza viongozi wa serikali kuhakikisha kuwa na namna yoyote ile, katika kufanya zoezi la utambuzi wa maeneo ya vijini na hifadhi ni sharti kuwa mbele maslahi makubwa wananchi – wafugaji .

2.5 Tunampongeza Mhe. Rais kwa tamko lake kwa kuweka bayana kuwa katika zoezi la kutambua na kweka mipaka baina ya maeneo ya hifadhi na vijiji au vitongoji ni sharti zoezi  hili liendeshwe kwa uwazi na kwa ushirikishwaji mkubwa sana wa wananchi -(wafugaji)

2.6 Tunampongeza Mhe. Rais kwa kuweka bayana kuwa zoezi hili lifanywe kwa haraka sana – kwa mwezi moja. Hii itaondolea taabu nyingi ambazo wafugaji wamekuwa wakiyapata kwa muda mrefu. Wananchi wanaopakana na maeneo yahifadhi kila  wakati wamekuwa na wasiwasi mwingikutokana  na  unyanyasaji unaofanywa dhidi yao na wahifadhi.

2.7 Tunampongeza Mheshimiwa Rais kuwa kuweka bayana kuwa kama kuna maeneo ya hifadhi ambayo yamepoteza hadhi ya uhifadhi kupewa wananchi – ( wafugaji) na kama ikibidi kubadilisha sheria iii kutoa maeneo hayo kwa wananchi- (wafugaji). Hili kwa kweli ni commitment kubwa sana ambayo haijawahi kutokea. Kwa miaka mingi wananchi ndio wamekuwa wanaondolewa kupisha uhifadhi. Mhe. Rais anatambua fika kuwa watu na mifugo inaongezekana, ardhi ni ile ile hivyo ni vyema sasa wahifadhi wetu wakatambua kuwa uhifadhi ni kwa maslahi ya wananchi kwa ujumla -na  pengine ni fursa kwa wahifadhi kuwa uhifadhi si kufukuza watu bali ni kushirikisha wananchi kikamilifu katika kuendeleza uhifadhi katika maeneo yao na wananchi kunufaika na uhifadhi huo.

 

3.0     WITO KWA WANANCHI – WAFUGAJI NCHINI

3.1 Sisi kama mashirika na viongozi wa wafugaji nchini tunatoa wito kwa wafugaji wote nchini kushirikiana na sisi katika kumpongeza Mhe. Rais na Serikali ya awamu ya Tano kwa kutambua changamoto wanazopata wafugaji nchini.

3.2 Sisi kama mashirika na viongozi wa wafugaji nchini tunatoa wito kwa wafugaji kutoa ushirikiano na kushiriki kikamilifu katika zoezi zima la kubaini maeneo yao katika zoezi kama ambavyo Mhe. Rais alivyoagiza na kutolea maelekezo kwa vyombo vya serikali.

Serikali kutambua kuwa uhifadhi mzuri ni pamoja na ushirikishaji wa wananchi-wafugaji kwa ajili ya ustawi wa uhifadhi endelevu na wenye kunufaisha wananchi.

4.6 Tunatoa wito kwa Wabunge na Bunge la Jamhuri ya Muungano kuhakikisha maagizo haya ya Mhe. Rais kuhusu wafugaji yanapewa kipaumbele na kufanywa kikamilifu na kwa nia njema aliyoionyesha Mhe. Rais katika kuwatetea wananchi wanyonge (wafugaji).

 

5. HITIMISHO:

Ndugu wanahabari tunapenda kuwajulisha kuwa siku ya jumamosi tarehe 19/1/2019 sisi kama mashirika na viongozi wa wafugaji nchini tumepanga kufanya maandamano ya makubwa AMANI ya kumpongeza Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kama ishara ya kuonyesha kufurahishwa kwetu na maagizo na maelekezo ya Mhe. Rais kwa vyombo vya serikali yenye nia njema na dhati ya kutetea wananchi (wafugaji) ambao kwa muda mrefu wamekuwa wananyanyashwa, kufukuzwa, kuchomewa mali na kutaifishwa mali zao katika maeneo yao wanayopakana na uhifadhi nchini.

Kwa hili tunadiriki kusema bila kuficha kuwa Mhe. Rais ametukuna wafugaji na kwamba ameonyesha dhahiri kuwa ni mtetezi wa wananchi wanyonge (wafugaji). Maandamano haya yatafanyika mjini Arusha. Tunanawakaribisha wote walioguswa na tamko la Mhe. Rais kuhusu wafugaji kushiriki katika maandamano haya ya Amani. Viongozi wetu wataendelea kuratibu maandamano haya na kuujulisha umma taratibu zote zikikamilika.

Karibuni wote. Asanteni kwa kutusikiliza.

 

Tamko hili limetolewa kwa niaba ya wafugaji nchini na wawakilishi na taasisi mbalimbali kutoka wilaya mbalimbali za Simanjiro, Kiteto, Ngorongoro, Longido, Siha, Hanang na Monduli kama ifuatavyo;

 

1.   Mhe. Mbunge wa Simanjiro -CCM, James Ole Milya

2.   Ujamaa Community Resource Team- (Ujamaa-CRT)

3.   PINGO’s Forum – Pastoralists Indigenous Non Governmental Organization’s Forum

4.   Pastoral Women Council – PWC

5.   Chama cha Wafugaji Tanzania

6.   Wawakilishi wa Vjiji Narakawo-Simanjiro

7.   Wawakilishi wa Kijiji cha Kimotorok-Simanjiro

8.   Diwani Kata ya Narakawo – CCM

9.   Wawakilishi kutoka Kijiji cha Terrat – Simanjiro

10. Wawakilishi kutoka – Kijiji cha Sakala – Ngorongoro

11. Wawakilishi kutoka Kijiji cha Makame – Kiteto

12. Wawakilishi kutoka Kijiji cha lrkiushibor – Kiteto

13. Wawakilishi kutoka Kijiji cha Emboreet- Simanjiro

14. Wawakilishi kutoka Kijiji cha Loiborsiret- Simanjiro

15. Wawakilishi kutoka Kijiji cha Oloirein – Ngorongoro

16. Wawakilishi  kutoka  Loolera -Kiteto

17. Wawakilishi kutoka Kijiji cha Loiborsoit- Simanjiro

18. Wawakilishi kutoka Kijiji cha Kirtalo-Ngorongoro

19. Wawakilishi kutoka Kijiji cha Mondorosi – Ngorongoro

20. Wawakilishi kutoka Kijiji cha Arash – Ngorongoro

21. Wawakilishi kutoka Kijiji cha Selela – Monduli

22. Wawakilishi kutoka Kijiji cha Mundarara – Longido

23. Wawakilishi kutoka Kijiji cha Malambo – Ngorongoro

24. Wawakilishi kutoka Kijiji cha Edony Ormurwak – SIHA

25. Wawakilishi kutoka Kijiji cha Simbay – Hanang